TAARIFA MPYA
MAMLAKA YA Chakula TFDA Yafungia kiwanda baada ya kutumia nembo isiyo sahihi
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), Kanda ya Kaskazini imekifungia kiwanda cha kampuni ya Derrick Global Trading Company Limited, kinachozalisha vinywaji aina ya Banana Wine baada ya kubainika kutumia nembo ya kiwanda kingine kinyume cha sheria.
Kiwanda hicho kilichopo mjini Moshi, kimefungwa kwa mara ya pili sasa, mara ya kwanza kilifungwa na serikali ya mkoa huo kutokana na kutokuwa na kibali halali cha uendeshaji wa biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkaguzi wa chakula kutoka TFDA, William Mhina, alisema wamekifunga kiwanda hicho baada ya Mamlaka hiyo, kufanya operesheni maalumu iliyofanikisha kubaini ukiukwaji huo wa sheria.
“Tumekuta kiwanda cha Derrick Global Trading Company Limited, wakiwa wanazalisha vinywaji vikali aina ya shujaa portable spirit, ambayo hatimiliki ya pombe hiyo ni ya kampuni nyingine,” alisema.
Alifafanua kuwa kampuni hiyo ilikutwa ikizalisha vinywaji hivyo wakati mmliki wa bidhaa hiyo ni kampuni ya Canon General Surprire Ltd ya mjini Shinyanga.
Alisema ni kinyume cha sheria mtu kuzalisha bidhaa ambayo leseni yake haimruhusu kutengeneza.
“Yeye amesajiliwa kutengeneza pombe aina ya Banana Wine, ambayo haina kilevi, lakini cha kushangaza tumekuta anazalisha spirit kwa kutumia nembo ya kampuni nyingine na anuani zote ni za kampuni ya Canon General Surprire Ltd,” alisema.
Aidha, alisema mamlaka hiyo imesitisha uzalishaji kiwandani hapo kutokana na miundombinu ya kiwanda hicho kutokuwa rafiki kiafya na kwamba wataruhusiwa kuendelea na uzalishaji tu pale watakapojirekebisha.
Ofisa Mwandamizi wa kodi wa TRA mkoani Kilimanjaro, Tilison Kabuje, alisema mamlaka hiyo ilifuatilia suala hilo baada ya kuona bidhaa ya Shujaa iko mitaani.
“Tulipokuwa tukifanya ukaguzi wa kawaida ndipo tukagundua ya kuwa bidhaa hiyo inazalishwa na Derrick Global Trading Co. LTD, kinyume cha sheria,” alisema.
Alisema katika uchunguzi huo walibaini ya kuwa bidhaa hiyo pia ilikuwa haina stempu halali ya TRA kutokana na iliyokuwapo kuwa ya bandia.
Meneja mauzo wa kampuni ya Canon General Surprire Ltd., kutoka mkoani Shinyanga, Laurent Chacha, walijulishwa na raia wema kuzalishwa kwa bidhaa hiyo mkoani Kilimanjaro, kinyume na sheria.
“Tulifuatilia suala hili na kugundua kweli bidhaa yetu ilikuwa inazalishwa visivyo halali na ndipo tukawasiliana na mamlaka husika, ikiwamo Jeshi la Polisi,” alisema.
Meneja wa Derrick Global Trading Co.Ltd Boniface Shee, alisema hayuko tayari kuzungumzia suala hilo kwa vile si msemaji wa kampuni hiyo.
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
Maoni
Chapisha Maoni
TAFADHARI !!
- Tumia Lugha Nzuri Kutoa Maoni
Usitumie kauli za Karaha AU Zenye Kukela :
C.E.O
Gneous OG