TAARIFA MPYA
SERIKALI yasema Haina Mpango wa Kuchoma Moto wala kuuza,
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
Dar es Salaam. Wakati China ikipiga marufuku biashara ya meno ya tembo, Serikali imesema haina mpango wa kuuza wala kuteketeza meno iliyonayo.
Kabla ya kuukaribisha mwaka mpya, Desemba 31, 2017, Waziri wa Misitu wa China, Zhang Jianlong alitangaza marufuku ya kuingiza nchini humo meno hayo kwa wafanyabiashara wote.
Kutokana na msimamo huo uliosubiriwa kwa muda mrefu, katibu mkuu wa Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema uamuzi huo utasaidia kupambana na ujangili nchini na Afrika kwa ujumla.
Kwa kutambua uwepo wa zaidi ya tani 118 za meno hayo nchini ambayo wakati fulani wadau waliishauri Serikali ama kuyauza au kuyateketeza, katibu mkuu huyo alisema yataendelea kutunzwa.
“Mpango wa kuyauza meno hayo kwa sasa haupo. Na hatutayateketeza, tutaendelea kuyatunza,” alisema meja jenerali huyo.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyoridhiwa mwaka 1975 na mataifa mbalimbali duniani chini ya mkataba unaopiga marufuku biashara ya wanyama na mimea iliyo hatarini kutoweka (Cites), nchi zote zinapaswa kuteketeza nyara inazokamata au ilizonazo ili kuvunja nguvu masoko ya vitu hivyo duniani.
Hazina ya meno hayo iliyopo, Meja Jenerali Milanzi alisema imetokana na makusanyo yaliyofanywa tangu miaka ya 1960 kutoka kwa tembo waliokufa, operesheni za kupunguza idadi ya tembo na nyara zilizokamatwa kutoka kwa majangili.
Tembo waongezeka
Alisema mikakati ya kupambana na ujangili inaendelea vizuri na tayari wizara hiyo imefanikiwa kuudhibiti kwa kiasi kikubwa.
“Hatujaumaliza lakini hali imebadilika. Mizoga ya tembo imepungua sana tofauti na ilivyokuwa zamani na tembo wameongezeka kidogo. Sasa hivi migogoro imeanza kujitokeza baina ya wananchi na tembo,” alisema.
Kutokana na ongezeko la wanyama hao kwenye hifadhi zilizopo nchini, migogoro kadhaa ilishuhudiwa wilayani Tunduru ambako tembo kutoka Hifadhi ya Selous walivamia mashamba na kuwashambulia wananchi.
Mkuu wa wilaya hiyo, Juma Homera alisema uongozi wao unajitahidi kuhakikisha madhara yanayotokana na ongezeko la tembo yanadhibitiwa kwa kushirikiana na wadau muhimu.
“Mwaka jana kulikuwa na vifo saba vilivyotokana na wanyama kuwashambulia wananchi. Tuliunda kikosikazi ambacho kuanzia Julai mwaka huo kimefanikiwa kudhibiti muingiliano uliokuwapo,” alisema Homera.
Kati ya waliouawa, Homera alisema wanne walivamiwa na tembo na waliobaki walishambuliwa na fisi. Wananchi waliopoteza maisha ni wa vijiji vya Rahaleo, Kajima na Twendembele.
Baada ya kuona madhara hayo, alisema kikosikazi maalumu cha kudhibiti uvamizi wa wafugaji kwenye hifadhi hiyo ya Taifa na kuzuia kutoroka kwa wanyama hao na kwenda vijijini kiliundwa.
Ili kupata suluhu ya kudumu, halmashauri hiyo iliiondoa mifugo yote iliyokuwa imeingizwa hifadhini na kupima vitalu 72 kwa ajili ya wafugaji kuendelea na majukumu yao. “Lilikuwa ni agizo la Waziri Mkuu. Tumelitekeleza na hali imetulia,” alisema Homera.
Licha ya jitihada hizo za ndani, mkuu huyo wa wilaya anashirikiana na Wilaya ya Miasa ya Msumbiji kudhibiti ujangili na uvunaji holela wa misitu.
Udhibiti wa ujangili
Kudhibiti ujangili na biashara ya meno hususan ya tembo, Kamati ya Okoa Tembo wa Tanzania imekuwa ikipaza sauti kutaka viumbe hao waendelee kupatiwa ulinzi madhubuti ili wasiangukie kwenye mikono ya majangili.
Kilio kikubwa cha kamati hiyo, wakati fulani kilikuwa kwa mataifa ya China, Singapore, Bangladesh na Thailand ikiyataka kuwabana wananchi wao wasiendeshe biashara hiyo na watunge sheria kali zitakazosaidia kuokoa tembo barani Afrika ambao wamekuwa wakilengwa na majangili wanaovutiwa na soko la nchi hizo.
Serikali miaka yote inapokamata nyara hizo imekuwa ikizihifadhi ghalani na kutumia fedha nyingi kuzilinda, ikielezwa hutumia zaidi ya Sh157 milioni kwa mwaka.
Maeneo mbalimbali nchini, Serikali imeendesha operesheni ya kuwaondoa wavamizi wa hifadhi za Taifa na mapori tengefu ili kuvilinda vivutio hivyo vya utalii kwa nia ya kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa.
Utekelezaji wa mpango huo umeenda sambamba na uvunjaji wa nyumba za wafugaji zilizojengwa ndani ya hifadhi hizo na kuwataka kuhamia vijijini ambako maeneo maalumu ya kufugia yametengwa.
China ilikuwa tishio
Baada ya jitihada zilizoanza mwaka 2015 China ilipochukua hatua ya kudhibiti biashara ya meno ya tembo, hatimaye mchakato huo umeonyesha kukamilika. Wakati jumuiya ya kimataifa ilipiga marufuku biashara hiyo mwaka 1990, China ilianza kuchukua hatua Februari 26, 2015 ilipotangaza mwaka mmoja wa kuzuia uagizaji wa pembe hizo na Desemba 31, 2016 ikazuia kabisa biashara hiyo. Jitihada hizo zimeshuhudia marufuku ikitolewa Jumapili iliyopita.
Mkuu wa Shirika la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori Duniani (WWF) nchini humo, Zhou Fei alisema amri hiyo ya Serikali itasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapambano dhidi ya ujangili.
Akizungumza na Shirika la Habari la Xinhua, Fei alisema: “Ni siku ya kihistoria. Ni uamuzi uliosubiriwa kwa muda mrefu. Hatimaye umetimia”
Hadi Machi, 2017, shirika hilo linasema maduka na viwanda 67 vya pembe hizo vilikuwa vimefungwa huku 105 vilivyobaki vikitarajiwa kufungwa Jumapili ya mwisho wa mwaka huo. Bei ya pembe ghafi imeshuka kwa asilimia 65 na kufikia Dola 1,100 za Marekani (zaidi ya Sh2.42 milioni) kwa kilo moja.
Bidhaa zinazotokana na pembe hizo pamoja na mambo mengine hutumika kuonyesha ufahari kwa anayezimiliki.
Mkurugenzi wa WWF Afrika, Dk Fred Kwame Kumah alisema zuio hilo litasaidia kuitokomeza biashara hiyo kutokana na kukosa soko la uhakika. Hata hivyo, kwa muda mrefu China ilizuia uuzaji wa pembe zilizopatikana baada ya mwaka 1975 kutokana na mkataba wa Cites.
Licha ya zuio hilo la Serikali, Jiji la Hong Kong bado linaruhusu biashara hiyo ingawa inaelezwa kwamba lipo mbioni kurekebisha sheria zake ili kuipiga marufuku mapema iwezekanavyo. Jiji hilo ni soko muhimu nchini China.
Ijumaa iliyopita, kampeni kubwa ya uelimishaji ilianzishwa nchini humo kwa ushirikiano wa wizara ya misitu, Chama cha Kuzuia Ujangili China (CWCA), WWF na Shirika la WildAid.
“Tunauanza mwaka 2018 tukiwa na matumaini kwamba tembo watakuwa salama baada ya China kuzuia biashara ya pembe zao, bei imeshuka na usimamizi wa sheria sehemu nyingi duniani umeongezeka,” alisema ofisa mkuu mtendaji wa WildAid, Peter Knights.
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
Maoni
Chapisha Maoni
TAFADHARI !!
- Tumia Lugha Nzuri Kutoa Maoni
Usitumie kauli za Karaha AU Zenye Kukela :
C.E.O
Gneous OG