TAARIFA MPYA
HAJI APATA MKATABA KENYA
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
Beki wa kushoto wa Yanga, Mwinyi Haji.
IMEBAINIKA kwamba uongozi wa timu ya AFC Leopards ya Kenya umemalizana na beki wa kushoto wa Yanga, Mwinyi Haji na umempa mkataba wa miaka miwili huku kinachosubiriwa kwa sasa ni beki huyo kupewa ruhusa na timu yake kabla ya kujiunga na timu hiyo ambayo inashiriki ligi ya Kenya.
AFC Leopards inayonolewa na Mtanzania, Dennis Kitambi, imefikia uamuzi huo wa kumpa mkataba beki huyo baada ya kukoshwa na uwezo wake aliouonyesha wakati akiwa na timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes wakati ilipokuwa inashiriki michuano ya Chalenji iliyofikia tamati hivi karibuni.
Chanzo cha karibu na beki huyo kimeliambia Championi Jumatatu kuwa Wakenya hao walishamalizana na Mwinyi ambapo kwa sasa kinachosubiriwa ni Yanga kumpa ruhusa beki huyo baada ya hivi karibuni kuandika
barua ya kutaka kuondoka kutokana na kukosa namba ndani ya kikosi cha kwanza.
“AFC Leopards wamefanya kweli baada ya kuonesha nia ya dhati tangu walipovutiwa na Mwinyi wakati akiwa na Zanzibar Heroes ambapo tayari wamempa mkataba wa miaka miwili wa kujiunga na timu hiyo, ambapo kwa sasa anasubiriwa yeye tu kwenda na kuanza maisha mapya.
“Ila ugumu umebaki kwa Yanga pekee ambapo kama wao wakikubali kumuachia kama yeye alivyoandika barua ya kuondoka hivi karibuni basi ataenda kujiunga na timu hiyo moja kwa moja, kinachosubiriwa kwa sasa ni Yanga kutoa ruhusa kwake ya kuondoka pekee lakini suala la kimkataba tayari wamemalizana,” kilisema chanzo hicho.
Hivi karibuni, uongozi wa Yanga kupitia kwa katibu wake mkuu, Charles Mkwasa, ulitoa tamko la kupokea barua ya beki wao, Mwinyi Haji ya kutaka kuondoka lakini pia waliwataka viongozi wa Leopards wawafuate kwa ajili ya kumalizana ili wamruhusu beki huyo.
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
Maoni
Chapisha Maoni
TAFADHARI !!
- Tumia Lugha Nzuri Kutoa Maoni
Usitumie kauli za Karaha AU Zenye Kukela :
C.E.O
Gneous OG