TAARIFA MPYA
VIGOGO WAPONZWA NA CHAPA
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
o
VIGOGO kadhaa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wameponzwa na zoezi la upigaji chapa mifugo nchi nzima, baada ya kuvuliwa nyadhifa zao.
Uamuzi wa kuwawajibisha vigogo hao umefanywa na waziri wa wizara hiyo, Luhaga Mpina, huku akiongeza muda wa mwezi mmoja zoezi la upigaji chapa mifugo kitaifa.
Waliovuliwa nyadhifa ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Erastus Mosha na Kaimu Mkurugenzi wa Ugani na Usajili, Bezia Rwengozibwa kwa kushindwa kusimamia kikamilifu zoezi hilo kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo na 12 ya mwaka 2010 na Kanuni zake za Mwaka 2011 GN 362.
Mbali na wakurugenzi hao, pia maofisa wawili wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Luzangi Deogratius na Felista Kimario ambao wamepewa onyo kali kwa kushindwa kusimamia zoezi hilo huku waliovuliwa madaraka akiagiza wachukuliwe hatua kali za kinidhamu.
Akizungumza jana katika zoezi la kuhitimisha upigaji chapa kitaifa katika Kata ya Migato Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, Waziri Mpina alisema kutokana na utekelezaji wa zoezi hilo kutokuwa la kuridhisha kwani asilimia 38.5 ya ng’ombe milioni 19,219,487 waliotakiwa kupigwa chapa ni ng’ombe milioni 7,401,661 tu ndio waliopigwa chapa tangu Desemba 14, 2016 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipoielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupiga chapa mifugo yote nchini ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji wa Mifugo na 12 ya mwaka 2010 na Kanuni zake za Mwaka 2011 GN 362.
Mpina alisema hadi kufikia jana Desemba 31 jumla ya ng’ombe milioni 7,401,661 sawa na asilimia 38.5 wamepigwa chapa ambapo kiasi cha Sh. bilioni 3.7 kwa malipo ya Sh. 500 kwa kila ng’ombe zilikusanywa huku Halmashauri 62 zikiwa zimepiga chapa kati ya asilimia 50 na 100, Halmashauri 43 wamepiga chapa kati ya asilimia 10 hadi 50, Halmashauri 23 wamepiga chapa chini ya asilimia 10 huku Halmashauri 30 zikiwa hazijaanza kabisa utekelezaji wa zoezi hilo, jambo ambalo amelitafsiri kama ni uzembe, kukaidi na kugoma kutekeleza zoezi hilo kulikofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali.
“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya Sheria ya Utambuzi, Usafiri na Ufuatiliaji wa Mifugo namba 12 ya mwaka 2010 na kanuni zake za mwaka 2011 G.N 362, ninaongeza muda wa kupiga chapa hadi tarehe 31 Januari 2018 katika kipindi hicho ng’ombe wote wawe wamepigwa chapa," alisema Mpina.
Mpina alisema haiwezekani tangu zoezi lianze hadi sasa halmashauri 30 hazijaanza huku halmashauri 23 zikiwa zimetekeleza chini ya asilimia 10, utaratibu dhaifu wa halmashauri ambapo tafsiri yake ni kukaidi utekelezaji wa sheria na maelekezo ya viongozi wakuu.
“Kutokana na udhaifu huu halmashauri zote 30 ambazo hazijaanza kabisa kupiga chapa na halmashauri 23 ambazo zipo chini ya asilimia 10 majina ya halmashauri hizo na majina ya viongozi wake nimeyapeleka kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi, kwani Serikali haiwezi kukubali mzaha wa aina hiyo katika usimamizi wa maagizo ya viongozi wakuu wa nchi,” alisema.
Aidha, Waziri Mpina alitaja changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa zoezi hili ni pamoja na kutambua na kuorodhesha wafugaji na idadi ya mifugo wanayomiliki, uhaba wa fedha wa kutoa elimu ya uhamasishaji na kutengeneza chapa kwa sababu haikuwamo kwenye bajeti 2016/2017, licha ya agizo hili ni la tangu Desemba 2016.
Pia changamoto nyingine ni kubaini mifugo kutoka nje ya nchi, wafugaji kutotaja idadi kamili ya mifugo waliyonayo, wafugaji kukataliwa kupigiwa chapa mifugo yao kwa kisingizio kuwa wavamizi au wahamiaji haramu hasa maeneo ya Rufiji, Kibiti, Sumbawanga, Tanganyika na Kibondo, kutofautiana gharama za uchangiaji wengine Sh. 500 wengine 1, 000 ni kinyume cha bei elekezi, fedha za kupiga chapa zinapokusanywa kupangiwa matumizi mengine badala ya chapa.
Hivyo Waziri Mpina aliamuru Halmashauri zote zilizotoza kiwango cha juu ya bei elekezi ya Sh. 500 wawarudishie wafugaji fedha zao haraka kabla hatua zaidi za kinidhamu hazijachukuliwa dhidi yao.
“Kwa kuwa sababu nyingine zilizotolewa na baadhi ya halmashauri kushindwa kutekeleza agizo hilo ni za msingi sana kama utambuzi wa mifugo na kwa kuwa hazijasababishwa na wafugaji ni wao hawajafikiwa na serikali kupigiwa chapa ni lazima ifikapo Januari 31 ng’ombe wote kote nchini wawe wamepigwa chapa,” alisema.
Mbunge wa Itilima, Njalu Daudi Silanga, alifikisha malalamiko ya wafugaji wa jimbo hilo ikiwamo kuendelea kunyanyaswa kwa kukamatwa na kupigwa mnada mifugo yao kwa kisingizio cha kuingia kwenye hifadhi jambo ambalo, Waziri Mpina alisema katika uongozi wake ndani ya Wizara hiyo halitaendelea tena.
- Pata kiungo
- X
- Barua pepe
- Programu Nyingine
Maoni
Chapisha Maoni
TAFADHARI !!
- Tumia Lugha Nzuri Kutoa Maoni
Usitumie kauli za Karaha AU Zenye Kukela :
C.E.O
Gneous OG